Watumiaji wa kilevi cha shisha (sheesha) wako katika hatari kubwa ya kuugua maradhi ikiwemo saratani na kuathirika katika mfumo wa hewa. Wataalamu wa afya wameonya kwamba ulevi huo ambao kwa sasa umeshika kasi na kuteka watu wengi hasa vijana, una hatari kubwa kuliko uvutaji wa sigara. Iinasadikiwa watu wengi, hususani vijana, hivi sasa wameibukia katika uvutaji huo, wakiamini ndiyo mbadala wa sigara kwa kudhani kuwa haina madhara. Daktari wa Kitengo cha Matibabu ya Saratani, Hospitali ya Aga Khan, Dk Amiyn Alidina, alisema hayo kwenye majadiliano ya ufahamu wa magonjwa ya saratani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Dk Alidina alisema kilevi hicho hakina tofauti na sigara, ambayo mvutaji wake hawezi kukwepa magonjwa ya saratani, maradhi ya moyo na maradhi ya mfumo wa hewa. “Shisha haiwezi kuwa mbadala wa sigara kwa kudhani kuwa mtu hawezi kupata saratani na magonjwa mengine, hii ni hatari zaidi,” alisema. Ulevi huo hutengezwa kwa kutumia chombo maalumu chenye bomba la kutolea moshi, a...